Conferences Wikia
Advertisement

Mkutano wa Wanablogu wa Tanzania ni mkutano wa kwanza rasmi wa wanablogu wa Tanzania ambao utafanyika katika mtandao wa tarakilishi, Intaneti, tarehe 18 Novemba, 2006.

Soma aliyoandika Jeff Msangi kuhusu mkutano huu kwa kubonyeza hapa

Nia ya ukurasa huu ni kuwezesha washiriki kuweza kujadili agenda muhimu za kujadiliwa na mambo mengine muhimu ili kuweza kufanikisha mkutano huu.

Saa[]

 1. Kura 22 zimepigwa kuchagua saa nane mchana kwa saa za Tanzania
 2. Kura 19 zimepigwa kuchagua saa sita mchana kwa saa za Tanzania
  • Hivyo: Mkutano wa wanablogu na wapenzi wa blogu wa Tanzania ni tarehe 18 Novemba, 2006, saa nane mchana saa za Tanzania.
 • Kama unataka kujua saa nane za mchana Tanzania ni saa ngapi hapo ulipo (kama upo nje ya Tanzania), bonyeza hapa

Muda wa Mkutano[]

 • Napendekeza saa mbili - Da'Mija
 • Naunga mkono - Ndesanjo
 • Naunga mkono - msangimdogo
 • naunga mkono - Mkwinda
 • Naunga mkono - Simbadeo


  • Kumbuka: mazungumzo baada ya habari yanaruhusiwa kufanyika baada ya mkutano!

Ukumbi wa Mkutano[]

Mkutano huu utafanyika kupitia teknolojia ya Internet Relay Chat, hivyo utakuwa ni mkutano wa mtandaoni. Bonyeza HAPA uende kwenye tovuti ya mkutano.

Maelezo: Maelezo haya ni muhimu sana maana usipoyafuata hutaweza kushiriki.

 1. Nenda kwenye tovuti ya IRC@Work (http://www.ircatwork.com/)
 2. Ukifika hapo utakuta kisanduku kina sehemu tatu.
 3. Sehemu ya kwanza inasema Nickname. Andika jina lako kwenye kisanduku hicho.
 4. Sehemu ya pili inaitwa Server. Usiandike chochote au kubadili chochote hapo
 5. Sehemu ya tatu inaitwa Channel, hapo utaandika: #blogubongo
 6. Baada ya kufanya hivyo, bonyeza pale panaposema Login
 7. Utakuwa umeingia ndani ya ukumbi wa mkutano.
 8. Ukishaingia, upande wa juu kulia utaona majina ya watu wengine walioko ukumbini. Ukitazama chini kabisa utaona ufito mwembamba ambao ndio utautumia kuandika mchango wako kwenye mkutano. Ukishaandika unabonyeza Enter kwenye kompyuta yako ili mchango wako usomwe.
  • Tafadhali fuata vyema maelezo haya.
  • Tafadhali tumia jina lako. Ni vyema tukafahamiana ili mtu akitoa wazo linalohitaji kufanyiwa kazi baadaye tuweze kuwasiliana naye iwapo tunahitahi ufafanuzi zaidi, ushauri, n.k.
  • Iwapo wewe hujulikani kwa wanablogu ni vyema utakapoingia ukajitambulisha. Unaweza kusema, "mimi ni fulani, ni msomaji wa blogu." Au "mimi ni fulani, nataka kuanza kublogu."

Msimamizi wa Mkutano[]

Ili mkutano uwe na mafanikio, ni vyema kukawa na msimamizi ambaye atahakikisha kuwa majadiliano yanafuata hoja iliyoko mezani. Ni jambo la kawaida kwa mikutano kuwa na wajumbe ambao wanaweza kuwa na hoja nyingi zilizo nje ya mada. Hivyo, ili kuhakikisha kuwa tunatumia muda wetu vyema, ni jambo zuri kukawa na msimamizi.

Jeff anampendekeza:

Naunga mkono pendekezo hili - ndesanjo

Naunga mkono - Da'Mija

Naunga mkono- Jeff

Naunga mkono - Miriam

Ajenda Rasmi[]

Hizi ni ajenda rasmi toka kwa msimamizi wa mkutano, Ramadhani Msangi. Unaweza kutoa mawazo yako kuhusu ajenda rasmi hizi. Mwisho wa kupokea mawazo ni saa nne asubuhi tarehe 18 Novemba, 2006 saa nne asubuhi kwa saa za Tanzania.

 1. LENGO
 2. MAADILI
 3. JUMUIYA/UONGOZI
 4. TUZO
 5. SIKU YA BLOGU, NA
 6. MENGINEYO.


UFAFANUZI:

1. LENGO.

Ajenda hii imependekezwa na watu kadhaa. Nimeona katika ajenda hii tunaweza kupitia mambo yafuatayo ya msingi:-

  Visheni na Madhumuni
  Kuongeza wasomaji
  Teknolojia rahisishi katika kublogu
  Hatimiliki na namna tutavyonufaika na kazi zetu
2. MAADILI.

Hapa tunaweza kugusia suala zima la maadili, uhuru, mipaka na wajibu wetu kama wanahabari huru. Tunaweza kuwa tuko huru sana kwakweli kama ilivyo lakini ni vyema tukajua kuwa UHURU BILA MIPAKA, SI UHURU BALI UTUMWA. Na pia tutalipitia Azimio la Dodoma kama ulivyopendekeza na kuona namna ya kuliboresha.


3. JUMUIYA/UONGOZI

Ajenda hii ni muhimu na kama ulivyopendekeza tutaangalia Madhumuni, Visheni, Muundo wa Jumuiya, Mfumo wa uongozi na Katiba ya Jumuiya. Haya ndio mambo ya msingi kwa ujumla katika ajenda hii.

Pia kuna suala la kuwa na muhtasari wa blogi za Kiswahili ama kwa wiki, mwezi au hata kila siku, mkutano wa ana kwa ana wa wanablogi wa kitanzania (na muda wa kufanyika), na pia suala la umri, lakini haya yote yaliyoko katika ayah hii, nadhani yatategemea sana kuundwa kwa Jumuiya maana hiyo ndio itakayoweka mikakati ya utekelezwaji wa haya yote. HATUWEZI KUJADILI SUALA LA KUWA TUNAIHITAJI AU LAA, kwasababu kutajwa kwake kama ajenda tayari kunamaanisha kuwa inahitajika.

 4. TUZO.

Agenda muhimu lakini fupi sana. Tunachotakiwa kujadili hapa ni kuwa tunahitaji tuzo katika utaratibu upi?, kwa maana ya makundi gani nikimaanisha kile wenye lugha zao wanaita categories, Zawadi (kama zitahitajika nk), mfumo wa kuteua,n.k . Suala la muda wa kutolewa nadhani itakuwa kila mwaka wakati wa siku ya wana-blogu wa kitanzania.

 5. SIKU YA BLOGU TANZANIA.

Tutakachokifanya hapa ni kukubaliana kuwa iwe inafanyika siku gani, wakati gani na mambo ya kufanyika.


 6. MENGINEYO

Kama ilivyokawaida, hapa pako wazi kwa ajili ya lisilokuwepo kupandishwa kupitia hapa, na litafanyiwa kazi kulingana na muda.

MWISHO WA KUSAHIHISHA NI SIKU YA MKUTANO SAA NNE ASUBUHI KWA SAA ZA TANZANIA.

Ajenda (Mapendekezo)[]

(Bonyeza hapo juu [sio kule juu kabisa, bali hapo juu upande wa kulia] panaposema "edit" kisha ushiriki kuchangia katika kuamua ajenda na masuala mengine muhimu kwa ajili ya mkutano huu).

 • Wakati ukipendekeza ajenda, kumbuka suala la muda.
 • Iwapo ajenda zilizopendekezwa tayari unaziunga mkono, ziandike katika mapendekezo yako ili tujue ni ajenda zipi ambazo watu wengi wangependa zizungumziwe.
 • Ukurasa wa ajenda unahusu ajenda ambazo unapendekeza. Iwapo una suala linalohusu mjadala, basi weka maoni yako kwenye kipengele kinachohusu majadiliano ambacho kiko chini ya ukurasa huu wa Ajenda.
 • Msimamizi wa Mkutano huenda ndiye atakuwa na wajibu wa kutazama ajenda zipi zinakubaliwa na wengi, kisha atangaze ajenda rasmi.
 • Taarifa: Kwa kuzingatia kuwa mapendekezo ya ajenda yamekuwa yakiendelea kutolewa na washikadau mbalimbali, kila mmoja akiwa na mawazo yake, na kwakuwa kuna kipengele muhimu cha kujali muda ambao tutakuwa ukumbini, nadhani msimamizi wa mkutano apewe mamlaka ya kuanzisha kona ya AJENDA RASMI, ambapo atachuja ajenda zote zilizoko na kisha kupendekeza ajenda rasmi. Nimesema kupendekeza sababu bado haitamaanisha kuwa amemaliza yeye, bali washikadau wote watashiriki pia katika kuboresha agenda hizo.


 AJENDA

1. Umuhimu wa Blogi kwa Watanzania kama jamii inayoinukia - Jeff Msangi

2. WanaBlogi wa Kitanzania: tulipotoka, tulipo na tunakoelekea - Macha

3. Mchango wa Blogi/WanaBlogi katika jamii ya Kitanzania (Jeff/Ndesanjo)

4. Maadili ya uandishi wa Mtandaoni (Makene/Mkwinda)

5. Teknolojia rahisi za kublogi (Ndesanjo)

6. Nafasi ya Blogi katika kujenga jamii wajibikaji na uongozi bora (...........)

7. Tuzo (wote)

8. Nakubaliana na mchango wa Da Mija & Ndesanjo kuhusu kuwa msimamizi wa mkutano. Kama kuna ambaye ana mawazo yatakayoniwezesha kuendesha usimamizi huo kwa ufanisi basi naomba tuwasiliane.

9. Suala la Jumuiya naliunga mkono kwa asilimia 100, kama ilivyo kwa suala la Tuzo


Kwanza kabisa naunga mkono ajenda zote 6 zilizopendekezwa hapo juu, naamini uchambuzi wa ajenda hizi ni mkusanyiko wa hoja mbalimbali kama zilivyotolewa na wadau mbalimbali wa mkutano wetu mkuu wa kwanza (nasisitiza). Nadhani kwa ajenda hizo tutakuwa tumepiga hatua kubwa zaidi katika kufanya jumuiya yetu kuwa makini na endelevu.

Nimeona na kukubaliana na wadau juu ya muda wa kuanza kwa mkutano wetu, lakini sijaona juu ya muda wa kumaliza!!!

Pia ninaomba tena na tena jamani wadau mwenye nakala laini (soft copy) ya AZIMIO LA DODOMA tafadhali naomba anitumie kwa anuani hii: dr_pori@yahoo.com, nipo mtandaoni mpaka saa 4 kamili usiku huu jamani kusubiri hilo azimio ambalo nadhani ni mwongozo tosha kabisa kwangu katika kufikia malengo (baadhi) ya mkutano huu.

Shime wanablogu Watanzania mkutano ni wetu sote na tusiuache atiii!!


1 AJENDA YANGU KUU NI MADHARA YA TEKNOLOJIA HII MPYA KATIKA BARA LA AFRIKA.

2 MWANABLOGGU ATAMBULIKE KATIKA KUTETEA WAJANE NA YATIMA.

3.BLOGU ITAMBULIKE KAMA KIOO CHA JAMII.

JAH LIVE.


Kwanza kabisa kabla ya kuzungumzia ajenda ningependa kuuliza: Sijui tunataka tukutane kwa muda gani. Saa moja? Masaa mawili? Nadhani jibu hili linategemea zaidi wale wanaotumia migahawa ya kulipia. Tuamue muda kwanza ndipo tuamue ajenda ziwe ngapi? Au tuchague ajenda kisha ndio tuamue tutakutana kwa muda gani?

Lakini kwakuwa ni mara ya kwanza tunakutana, nashauri tusiwe na ajenda nyingi sana. Kwa mfano ajenda ya maadili (aliyopendekeza Msangi Mdogo) naona ni muhimu sana. Kingine ni kuwa badala ya ajenda kuwa chini ya baadhi ya watu kama alivyopendekeza Msangi Mdogo, ningependekeza ajenda ziwe wazi kwakuwa hakuna mtu atakayekuwa akitoa mada bali wote tukijadili kwa wakati mmoja.


Ajenda (ndesanjo):

1. Maadili (kama alivyopendekeza Msangi) (mjadala huu unaweza kugusia pia Azimio la Dodoma na umuhimu wa kulipanua na kulipa nguvu zaidi na taratibu za kutumika)

2. Jumuiya: je tunahitaji jumuiya rasmi? Nini madhumini yake? Muundo wake? Uongozi?

3. Tuzo (kama alivyopendekeza Msangi na Da'Mija)

4. Siku ya blogu Tanzania (kama alivyopendekeza Da'Mija)

Naunga mkono:

 • Naunga mkono ajenda ya Da'Mija ya Uongozi (ajenda alizopendekeza ziko hapo chini), ningependekeza ijumuishwe na ajenda kuhusu jumuiya niliyoitoa hapo juu (na maswali matatu makuu ambayo yanaweza kuongoza ajenda hiyo.
 • Pendekezo la Tuzo la Msangi Mdogo na Da'Mija nalo naunga mkono
 • Pia naunga mkono mkutano kuwa masaa mawili.
 • Pia wazo la kuwa na siku ya Blogu Tanzania. Hili ni wazo zuri sana hasa kama tuna nia ya kuhamasisha watu wengi zaidi kutusoma na kuwa na blogu zao.
 • Kwa mtazamo wangu mkutano huu kwakuwa ni wa kwanza, nadhani utakuwa na mafanikio iwapo utakuwa na ajenda ambazo nia yake ni kutupeleka kwenye kuwa na jumuiya na kuwa na msingi fulani wa maadili (ingawa tunaheshimu haki na uhuru wa kujieleza).
 • Ajenda ya Luihamu ya "Blogu itambulike kama kioo cha jamii" na pia blogu kutambulika kutetea yatima na wajane, pengine hizi zinaweza kuingia katika mjadala wa mada ya siku ya blogu Tanzania ambapo siku hiyo inaweza kuwa na madhumuni au ujumbe kama huo. • Napendekeza mkutano uwe wa masaa mawili.
 • Naunga mkono pendekezo kwamba Msangi Mdogo awe msimamizi wa mkutano.

1. Nakubaliana na ajenda ya 'Umuhimu, mchango na nafasi ya blogu katika Tanzania.

2. Nakubaliana na Tuzo, ila tujadili iwe inatolewa kwa kila baada ya muda gani.

3. Uwezekano wa kuwa na muhtasari wetu wa nini kilichojiri katika blogu zetu watanzania ila tupange muhutasari huo uwe kila baada ya juma au mwezi. (Suala la jumuiya hapa nadhani ndiyo mahala pake)

4. Kuunda siku ya blogu Tanzania, na kupanga kuwa na mkutano wa ana kwa ana japo kwa mwaka( hii iwe ni lazima).

5. Uongozi.5. Mawazo yote yaliyochangiwa ni muhimu, ila tuangalie namna gani wanablog wanaweza kunufaika na mtandao na mustakabali wake kwa vizazi vijavyo ni muhimu kupata muda wa kujadili hili ikiwa ni pamoja na kuzingatia maadili ya uandishi wa mtandaoni kwani hakuna udhibiti wa utoaji wa taarifa katika blog kwani kila mtu hujisemea awezavyo.

Pia tuangalie wanablog wameweza kufikisha ujumbe kwa watumiaji wa mtandao ipasavyo? hilo liangaliwe ikiwa ni pamoja na kuongeza ushawishi wa wasomaji wa blog hususan viongozi wa vyama vya siasa, wabunge, wahariri wa vyombo vya habari, waandishi na wananchi hususan watumiaji wa mtandao.

Hivyo mada ninazopendekeza ni:

 1. Maadili
 2. Namna wanablogu wanaweza kufaidika na teknolojia hii
 3. Jinsi ya kuongeza ushawishi kwa wasomaji wa blogu (hasa wabunge, wahariri, waandishi, wanasiasa, n.k.)Mchango wa Simbadeo:

Nafurahi kuona kuwa mkutano tayari ushaanza ingawa siyo rasmi kabisa. Umekwishaanza katika harakati hizi za kupendekeza ajenda. Kimsingi, naona kuwa ajenda karibu zote zilizopendekezwa ni nzuri na za maana sana. Hata hivyo, naunga mkono zaidi hizo zilizotajwa hapo juu:

 1. Maadili (Nafasi ya maadali katika matumizi ya blogu katika kiwango ambacho hakiathiri uhuru wa kujieleza na kuumiza wengine pasipo sababu).
 2. Namna gani watu tunaweza kufanya blogu tunazoanzisha kusomwa na watu wengi zaidi.
 3. Namna ya kulinda haki za waandishi wa blogu (hasa kuepa matumizi yasiyoidhinishwa ya yale yaliyo katika blogu), yaani hakimiliki na haki shirikishi (copyright and neighbouring rights).

Muda wa mkutano ninaunga mkono pendekezo la saa mbili (niwakumbushe tu kuwa siyo masaa mawili). Naamini sisi watumiaji wa internet cafe tutamudu gharama ya muda huo wa saa mbili.Naona ajenda muhimu zimeshawekwa na wengine. Nazipa kipaumbele ajenda zifuatazo:

 • Maadili.
 • kuundwa kwa jumuiya.
 • siku ya blogu za Tanzania
 • Tuzo

Pengine pamoja na kuafiki ajenda hizo, ningependa tufikirie picha ya mbali au lengo la kuu la jumuiya hiyo. "vision"

Ikesha juu ya uongozi, ni vyema tufikirie juu ya mfumo mzima wa kublogu ambao umetoa uhuru kwa wote kuandika wanachotaka bila kukinzwa na vyombo vilivyokuwa na "uongozi". Uongozi au usimamizi wa namna ipi utakaoweza kuendeleza uhuru uliopo sasa wakati ukitimiza lengo kuu "vision" ya jumuiya itakayoundwa.

Tutajadili zaidi mkutanoni.Kwa sababu hii ni mara ya kwanza kukutana, nadhani tungekuwa na ajenda chache. Tuwe focused. Kwa mtazamo wangu, tungekuwa na ajenda kuu tatu, ambazo wengi mmezigusia tayari:

 • Lengo letu - Najua kila mtu ana malengo ya kublog. Lakini kuna uwezekano tunakaja na "vision" au mwelekeo wa pamoja kutoka kwenye huu mkutano wa kwanza.
 • Maadili - Kama tutakubaliana juu ya malengo yetu ya pamoja, then maadili ni kitu cha kuweka "guidelines" za kuweza kufikia malengo hayo.
 • Tuzo - Ndio tuna blog, lakini lazima kuwepo na ubora fulani.

Napendekeza agenda ya siku za usoni, aidha kwenye mkutano kama huu au "discussion board":

 • Mkakati wa kuongeza ufanisi wa blog zetu - 1)kuongeza usomaji wa blog zetu 2) kuleta mabadiliko katika jamii etc


Na tuanze 'the count-down to that great day of Tanzania Blogging'.


Naomba moja ya ajenda iwe ni jinsi gani wanafunzi (toka msingi hadi chuo) watakavyoweza kuhamasishwa kujiunga na mtandao wa blogu, kwani idadi yao inaweza kuwa changamoto kwa wanachama.

Pia ningependa kuwepo na uchaguzi rasmi wa viongozi wa mtandao wa blogu za watanzania. napendekeza nafasi ziwe Mlezi, Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri wa wizara ambazo napendekeza ziundwe. Siku ya mkutano tutangaze hilo na pia tarehe ya uchaguzi ambayo napendekeza iwe mwakani, ili watu wajitokeze, wajinadi na kupiga kampeni.

Isisahaulike kwamba kwenye kitu kama hiki lazima iwepo na katiba ya kutuongoza. hivyo tuliwa twaelekea huko, katika itungwe, ijadiliwe na kisha iafikiwe kabla ya kupitishwa kwa kura.

Naomba kutoa hoja. AJENDA nazopendekeza ni:

 1. Jinsi ya kuhamasisha wanafunzi kujiunga na mtandao wa blogu
 2. Uchaguzi wa viongozi (mlezi, rais, makamu wa rais, waziri mkuu na mawaziri wa wizara mbalimbali. Uchaguzi huo ufanyike mwakani na kuwepo na kampeni)
 3. Kutungwa kwa katiba


 • Mchango wa Poli(aliyeko pichani kulia):
  Image021

  Poli katika e-kongamano

Napendekeza pia kujadiliwa kwa suala la namna ya kuwasaidia wanablogu wachanga jinsi ya kuboresha blogu zao na pia mafunzo kwa njia ya mtandao (e-learning) ili kuwa na jumuiya ya mtandaoni (e-community)iliyotengemaa.


Mimi napendekeza tukubaliane umri wa mwanachama. Nafikiria tusikubali wanachama chini ya miaka 18 au 21. Hii ni kwa sababu ya usalama wao, na pia kukinga jina la wanablogu wa Tanzania.

Majadiliano[]

 • Ushauri wa Ras Luihamu:

Ushauri wangu,tufanye kazi kwa kutegemeana na kupendana,tusiulize kwa nini MSANGI MDOGO kachaguliwa,cha msingi tufanye kazi kwa kutegemeana.Sisi Waafrika lazima utakuta baadhi ya wanablogu watalalamika kwa nini majina yao hayakupendekezwa,lakini cha msingi tufanye kazi kwa bidii na kupendana,blogu iwe kama familia moja ya baba mmoja na mama mmoja.Kuhusu AJENDA katika mkutano,kama narudia tena kama baadhi ya AJENDA zitakuwa zimeachwa naomba tuvumiliane na kufanya kazi,tusianze kuuliza kwanini ajenda yangu haikuchaguliwa.Nawaomba wanablogu tuheshimu,MUDA,SIKU,NA KUTUMIA LUGHA SAFI WAKATI WA MKUTANO.SIKU YA MKUTANO TUSIONGEZE AJENDA MPYA TENA TUHESHIMU AJENDA ZILIZO CHAGULIWA.

Naomba kuwakilisha ushauri wangu hata bila kupewa mamlaka ya kuandika ushauri.

 • ndesanjo anasema:

Luihamu nakubaliana nawe kabisa kuwa suala la msingi ni kufanikisha mkutano. Nani kauliza kwanini Msangi Mdogo kachaguliwa? Uwanja uko wazi kwa mtu yeyote kupinga pendekezo la jina lake na pia watu wengine kutoa mapendekezo. Sidhani kama jina lake tu ndio lina haki ya kupendekezwa.

Kuhusu ajenda: najua hakuna ajenda rasmi bado, hivi sasa tunabangua bongo ili kupata ajenda za msingi na pia kujua tutakutana kwa muda gani. Hivyo hakuna ajenda hata moja ambayo imeshakuwa ajenda rasmi. Ajenda zote zilizopendekezwa hadi sasa ninaziona kuwa ni muhimu sana. Ila kwakuwa hatukutani siku nzima, naona lazima tuchague ajenda ambazo zitatusaidia kujenga jumuiya kisha ajenda nyingine zitajadiliwa kwenye mikutano ijayo. Halafu kuna ajenda ambazo zinaingiliana, kwa mfano ajenda ya kuwa na Siku ya Blogu Tanzania kwa namna fulani inaendana na ajenda ya blogu kama kioo cha jamii. Blogu kama kioo cha jamii, kwa mfano, inaweza kuwa ni ujumbe wa siku ya blogu Tanzania. Kitu kama hicho. Lakini yote haya ni tisa, kumi ni majadiliano. Tujadiliane. Naona wengi tumekaa kimya sana.

 • msangimdogo anasema:

Raha ya teknolojia hizi ndio hii, mtu unaanzisha kitu ambacho kinakuwa na umuhimu hata wengine walikuwa hawajui. Ndesanjo alipoanzisha ukurasa huu msingi wake ulikuwa kuanzisha au kupendekeza ajenda za mkutano, lakini ona kumekuwa na kona nyingui ambazo kila moja ina umuhimu kwa ajili ya kufanikisha mkutano huu mfano hii ya majadiliano.

Kuna jambo naliona hapa, nalo ni ushiriki haba wa wahusika wa mkutano huu. Kuna watu wengi kwa ujumla ambao nikitaka kuwataja hapa nadhani nitajaza ukurasa, ambao hatujawaona ama kwenye kupendekeza muda, kuunga mkono wazo au hata kupendekeza ajenda, lakini niwaambie kitu kimoja ndugu zangu. DAIMA MWANZO NI MGUMU. NA SIO WENGI WALIOTAYARI KUTHUBUTU KWENYE JAMBO JIPYA.

Kama alivyosema Ndesanjo, Blogi sio upepo wa kupita na wengi wetu tunaona hili. Inawezekana kabisa kuwa katika hatua hizi za mwanzo tukawa na taabu kidogo katika jambo hili lakini ni vyema tujue kuwa sisi ambao tayari tumeshajitoa katika kutekeleza jambo hili, tuna jukumu kubwa sana la kuhakikisha kuwa tunaweka msingi wa blogi kama kitu tegemeo katika nchi yetu.

Tutumie kila mmoja wakati wetu kuwashawishi wale tunaoweza kuwashawishi washiriki katika jambo hili, lakini ikishindikana, basi sisi tuliothubutu, tuonyeshe kuwa tunaweza, tuonyeshe kuwa inawezekana na hatimaye matunda yake tutayaona.

 • ndesanjo anasema:

Kweli kabisa Msangi Mdogo. Teknolojia hii baadhi wanaweza wakaiangalia kimchemchezo. Ustaarabu, maendeleo, na utamaduni hujengwa juu ya Maarifa, Habari, na Elimu. Hivyo basi zana zinazotumika kuzalisha, kusambaza, kutunza Maarifa, Habari, na Elimu sio zana za kuzitazama kimchezomchezo. Mapinduzi hasa ya teknolojia hizi tunazotumia huenda tusiyaone sisi wakaja kuyaona wale wa vizazi vijavyo. Tunachofanya ni kuandaa njia na kuweka misingi. Hii ni kazi muhimu sana. Nyumba ikiwa na madirisha, mabati, milango, na sakafu nzuri lakini msingi wake ukawa mbovu itaanguka tu. Kwahiyo nakubalina nawe kuwa tuna jukumu la kuhakikisha kuwa tunaweka misingi dhabiti.

Wakati tukiweka hii misingi kuna mambo mengi tunaweza kujifunza bila hata kutambua. Kwa mfano, hivi sasa tunajifunza juu ya demokrasia shiriki ya mtandaoni. Hili ni jambo jipya kabisa kwenye historia ya mwanadamu. Tunafanya maandalizi toka A hadi Z ya mkutano kupitia mtandaoni bila kukutana ana kwa ana wala gharama kubwa, bila kuhitaji posho za chai ya saa nne. Hakuna anayedai mshiko. Hakuna kutafuta fedha za kukodisha ukumbi na mambo kama hayo. Tunayojifunza huku mtandaoni yanawezekana kabisa kuhamishiwa katika maisha ya ana kwa ana. Moja kubwa likiwa ni hili la demokrasia shiriki. Haya, kufupisha ninachosema: tusipoteze nafasi tuliyonayo kujenga misingi dhabiti ya teknolojia tunazotumia ili ziwe na manufaa kwa jamii nzima. Tushiriki!

 • Miriam anasema*

Nakubali ajenda yeyote msimamizi atakayozungumzia. Lakini napenda tukubaliane kuwa watoto wa msingi au chini ya miaka 18 wasiruhusiwe kuwa wanachama. Hii ni kwasababu ya usalama wao.

Habari Kuhusu Mkutano[]

Mapendekezo ya Wanablogu[]

 • Kwakuwa mkutano haukufikia muafaka masuala mbalimbali, mjadala kuhusu masuala hayo unaendelea na utaratibiwa rasmi na kamati ya muda inayoundwana Da'Mija, Jeff Msangi, ndesanjo macha, na Ramadhani Msangi.

Mapendekezo yaliyoandikwa katika blogu za wanajumuiya:


Blogu ya Kukusanya Maoni na Kujadili[]

Ili kufanikisha lengo ka kazi hii, kamati ya muda imeaandaa blogu ya kwa ajili ya kukusanya maoni na kujadili masuala kadhaa. Itembelee upate habari zaidi. Anuani yake hii hapa: http://www.blogutanzania.blogspot.com/ Au bonyeza hapa

Viungo[]

Advertisement